TAHARIRI
“Tazameni ni kwa herufi gani kubwa
nimewaandikia kwa mkono
wangu mimi mwenyewe”
(Wagalatia 6:11)
Na Frt. Richard Lusaluwa
Mtume Paulo anakazia kwamba yale yote aliyoyaandika aliandika kwa mkono wake mwenyewe na hakuna sababu ya kutilia mashaka huo ujumbe wake. Basi nasi ndugu zenu Waseminari wa Seminari Kuu ya Mwenye Heri Yosefu Allamano hapa Morogoro tunawakaribisheni tena kukisoma Kijarida hiki tulichokiandika kwa mikono yetu wenyewe tukilenga hasa kukuletea upembuzi wa mambo mbalimbali yanayotugusa sisi kama binadamu katika mfumo mzima wa maisha yetu ya kila siku; Kiroho, Kimwili na Kiakili. Lengo ikiwa ni kubadilishana Mang’amuzi na Ushauri, pamoja na kujifunza zaidi.
Tukiwa tunakaribia kufunga mwaka wa masomo na malezi hapa Seminarini 2011/2012, tunawaletea pia Matukio mbalimbali yaliyotukia katika Nyumba yetu ya Malezi. Tukilenga hasa kukujuza wewe msomaji wetu makuu ya Mungu anayoendelea kutukirimia sisi ndugu zenu hapa Morogoro.
Tunatoa shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya uhai na Wito pamoja na mapaji anayoendelea kutukirimia wana Jumuia na Shirika kwa ujumla. Tunamshukuru sana Baba Gombela na timu nzima ya Walezi kwa msaada wao wa hali na mali katika kufanikisha Jarida hili. Shukrani zaidi ziwaendee Waseminari wote kwa michango yao ya kiufundi na Ushauri katika kuhakikisha Jarida hili linakufikia wewe msomaji wetu. Mwisho tunawashukuru wafanyakazi wote katika nyumba hii kwa mchango wao, Mungu awarudishie.
Karibuni nyote.
No comments:
Post a Comment